Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: 2 Thessalonians

1:1 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.

1:2 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

1:3 Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.

1:4 Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.

1:5 Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka.

1:6 Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,

1:7 na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu

1:8 na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.

1:9 Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,

1:10 wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.

1:11 Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.

1:12 Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

2:1 Sasa yahusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanywa kwetu pamoja tukae naye. Ndugu, tunawaombeni sana

2:2 msifadhaike upesi moyoni, na wala msitiwe wasiwasi kwa sababu ya madai kwamba Siku ya Bwana imekwisha fika. Labda inadhaniwa kwamba jambo hili limetokana na uaguzi fulani, mahubiri au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu.

2:3 Msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa namna yoyote ile. Maana Siku hiyo haitakuja mpaka kwanza ule Uasi Mkuu utokee na yule Mwovu aonekane ambaye mwisho wake ni kuangamizwa kabisa.

2:4 Yeye atapinga kila kitu wanachokiona watu kuwa ni mungu, au wanachokiabudu. Naam, hata ataingia na kuketi ndani ya Hekalu la Mungu akijidai kuwa Mungu.

2:5 Je, hamkumbuki kwamba niliwaambieni haya yote wakati nilipokuwa pamoja nanyi?

2:6 Lakini kuna kitu kinachomzuia sasa, nanyi mwakijua kitu hicho. Basi, huyo Mwovu ataonekana wakati wake ufaao.

2:7 Hata hivyo, Mwovu huyo aliyefichika anafanya kazi sasa, lakini hataonekana mpaka yule anayemzuia aondolewe.

2:8 Hapo ndipo Mwovu atakapotokea; lakini Bwana Yesu anapokuja atamuua kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kwa mng'ao wa kuja kwake.

2:9 Huyo Mwovu atakuja na nguvu za Shetani na kufanya kila namna ya miujiza na maajabu ya uongo,

2:10 na kutumia udanganyifu wa kila namna kwa wale walio katika mkumbo wa kupotea. Hao watapotea kwa sababu hawakuupokea na kuupenda ule ukweli ili waokolewe.

2:11 Ndiyo maana Mungu amewaweka chini ya nguvu ya upotovu, wauamini uongo.

2:12 Matokeo yake ni kwamba wote wasioamini ukweli, ila wafurahia dhambi, watahukumiwa.

2:13 Tunapaswa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi ndugu, ninyi mnaopendwa na Bwana, kwa maana Mungu amewateua tangu mwanzo mpate kuokolewa kwa nguvu ya Roho mfanywe watu wake watakatifu kwa imani yenu katika ukweli.

2:14 Mungu aliwaitieni jambo hili kwa njia ya Habari Njema tuliyowahubirieni; aliwaiteni mpate kupokea sehemu yenu katika utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

2:15 Basi, ndugu, simameni imara na zingatieni yale mafundisho tuliyowafundisheni kwa mahubiri yetu na barua zetu.

2:16 Tunamwomba Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu ambaye alitupenda, na kwa neema yake akatujalia faraja ya milele na tumaini jema,

2:17 aifariji mioyo yenu na kuwaimarisheni ili mweze daima kutenda na kusema yaliyo mema.

3:1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili ujumbe wa Bwana uzidi kuenea upesi na kupokelewa kwa heshima kama vile ulivyo kati yenu.

3:2 Ombeni pia ili Mungu atuokoe na watu wapotovu na waovu, maana si wote wanaoamini ujumbe huu.

3:3 Lakini Bwana ni mwaminifu. Yeye atawaimarisheni na kuwalinda salama na yule Mwovu.

3:4 Naye Bwana anatupatia tumaini kubwa juu yenu, na hatuna shaka kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaambieni.

3:5 Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika uvumilivu tunaopewa na Kristo.

3:6 Ndugu, tunawaamuru kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, mjiepushe na ndugu wote walio wavivu na ambao hawafuati maagizo tuliyowapa.

3:7 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mnapaswa kufuata mfano wetu. Sisi tulipokuwa nanyi hatukuwa wavivu;

3:8 hatukula chakula kwa mtu yeyote bila ya kumlipa. Tulifanya kazi kwa bidii na taabu mchana na usiku ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote kati yenu.

3:9 Tulifanya hivyo si kwa kuwa hatuna haki ya kutaka msaada wenu, ila kwa sababu tunataka kuwapeni mfano.

3:10 Tulipokuwa pamoja nanyi tulikuwa tukiwaambieni, "Mtu asiyefanya kazi, asile."

3:11 Tunasema mambo hayo kwa sababu tumesikia kwamba wako baadhi yenu ambao ni wavivu na ambao hawafanyi chochote, isipokuwa tu kujiingiza katika mambo ya watu wengine.

3:12 Kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo tunawaamuru na kuwaonya watu hao wawe na nidhamu na kufanya kazi ili wajipatie maslahi yao wenyewe.

3:13 Lakini ninyi ndugu, msichoke kutenda mema.

3:14 Huenda kwamba huko kuna mtu ambaye hatautii huu ujumbe tunaowapelekeeni katika barua hii. Ikiwa hivyo, basi, mfichueni mtu huyo na msiwe na uhusiano wowote naye kusudi aone aibu.

3:15 Lakini msimtendee mtu huyo kama adui, bali mwonyeni kama ndugu.

3:16 Bwana mwenyewe ndiye chanzo cha amani, awajalieni amani siku zote kwa kila namna. Bwana awe nanyi nyote.

3:17 Kwa mkono wangu mwenyewe naandika hivi: Salamu kutoka kwa Paulo! Hivi ndivyo ninavyotia sahihi kila barua; ndivyo ninavyoandika.

3:18 Tunawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.


Next: 1 Timothy