Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Previous  Next 

Swahili Bible: Ephesians

1:1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu.

1:2 Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.

1:3 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni.

1:4 Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake,

1:5 Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia.

1:6 Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu katika Mwanae mpenzi!

1:7 Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake

1:8 aliotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote

1:9 Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo.

1:10 Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo.

1:11 Kila kitu hufanywa kufuatana na mpango na uamuzi wa Mungu; naye Mungu ametuteua sisi tuwe watu wake kwa mapenzi yake katika kuungana na Kristo, kufuatana na azimio alilofanya tangu mwanzo.

1:12 Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu!

1:13 Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonyesha kuwa ninyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia.

1:14 Huyu Roho ni dhamana ya kurithi yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!

1:15 Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu na mapendo yenu kwa watu wa Mungu,

1:16 sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu

1:17 ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua.

1:18 Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake,

1:19 mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu, ni sawa na nguvu ile kuu mno

1:20 aliyomfufua nayo Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni.

1:21 Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao.

1:22 Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote.

1:23 Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.

2:1 Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu.

2:2 Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu.

2:3 Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.

2:4 Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,

2:5 hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa.

2:6 Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.

2:7 Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu.

2:8 Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.

2:9 Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

2:10 Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

2:11 Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine--mnaoitwa, "wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita, "Waliotahiriwa," (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) --kumbukeni mlivyokuwa zamani.

2:12 Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani.

2:13 Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.

2:14 Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui.

2:15 Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.

2:16 Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu.

2:17 Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.

2:18 Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja.

2:19 Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu.

2:20 Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi.

2:21 Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana.

2:22 Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

3:1 Kutokana na hayo, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu, namwomba Mungu.

3:2 Bila shaka mmekwisha sikia kwamba Mungu, kwa neema yake, alinikabidhi kazi hii niifanye kwa faida yenu.

3:3 Mimi nilijulishwa kwa njia ya ufunuo mpango wake uliofichika. (Nimeandika kwa ufupi juu ya jambo hili,

3:4 nanyi mkiyasoma maneno yangu mtaweza kujua jinsi ninavyoielewa siri hiyo ya Kristo.)

3:5 Zamani watu hawakujulishwa siri hiyo; lakini sasa Mungu amewajulisha mitume na manabii wake watakatifu kwa njia ya Roho.

3:6 Siri yenyewe ni hii: kwa njia ya Habari Njema watu wa mataifa mengine wanapata sehemu yao pamoja na Wayahudi katika zile baraka za Mungu; wao ni viungo vya mwili uleule, na wanashiriki ahadi ileile aliyofanya Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

3:7 Mimi nimefanywa kuwa mtumishi wa Habari Njema kwa neema ya pekee aliyonijalia Mungu kwa uwezo wake mkuu.

3:8 Mimi ni mdogo kuliko watu wote wa Mungu; lakini amenijalia neema yake, ili niwahubirie watu wa mataifa utajiri wake Kristo usiopimika,

3:9 tena niwaangazie watu wote waone jinsi mpango wa Mungu uliofichika unavyotekelezwa. Mungu aliye Muumba wa vitu vyote alificha siri hiyo yake tangu milele,

3:10 kusudi, sasa kwa njia ya kanisa, wakuu na wenye enzi wa mbinguni wapate kuitambua hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi.

3:11 Mungu alifanya jambo hilo kufuatana na azimio lake la milele ambalo amelifanya kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

3:12 Basi, katika kuungana na Kristo, na kwa njia ya imani katika Kristo, sisi tunathubutu kumkaribia Mungu kwa uhodari.

3:13 Kwa hiyo, nawaombeni msife moyo kwa sababu ya mateso ninayopata kwa ajili yenu, maana hayo ni kwa ajili ya utukufu wenu.

3:14 Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba,

3:15 aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni.

3:16 Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu,

3:17 naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo

3:18 kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina.

3:19 Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu.

3:20 Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu, aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria;

3:21 kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.

4:1 Basi, mimi niliye mfungwa kwa kuwa namtumikia Bwana, nawasihi muishi maisha yanayostahili wito mlioitiwa.

4:2 Muwe daima wanyenyekevu, wapole na wenye saburi; vumilianeni ninyi kwa ninyi kwa mapendo.

4:3 Fanyeni bidii ya kuhifadhi umoja uletwao na Roho kwa kuzingatia amani iliyo kati yenu.

4:4 Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile tumaini mliloitiwa na Mungu ni moja.

4:5 Kuna Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja;

4:6 kuna Mungu mmoja na Baba wa wote, ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote.

4:7 Kila mmoja wetu amepewa neema kadiri ya kipimo alichojaliwa na Kristo.

4:8 Kama yasemavyo Maandiko: "Alipopaa mbinguni juu kabisa, alichukua mateka; aliwapa watu zawadi."

4:9 Basi, inaposemwa: "alipaa juu," ina maana gani? Maana yake ni kwamba, kwanza alishuka mpaka chini kabisa duniani.

4:10 Basi, huyo aliyeshuka hapa duniani, ndiye aliyepaa juu ya mbingu zote apate kuujaza ulimwengu.

4:11 Ndiye aliyewapa watu zawadi: wengine aliwajalia wawe mitume, wengine manabii, wengine wawe waeneza Habari Njema, wengine wachungaji na walimu.

4:12 Alifanya hivyo apate kuwatayarisha watu wote wa Mungu kwa ajili ya kazi ya huduma ya Kikristo ili kuujenga mwili wa Kristo,

4:13 na hivyo sote tuufikie umoja wa imani na kumjua Mwana wa Mungu; tuwe watu waliokomaa na kuufikia utimilifu wake Kristo mwenyewe.

4:14 Basi, hatutakuwa tena kama watoto, tukitupwa na kupeperushwa huko na huko kwa kila upepo wa mafundisho wanayozua watu wadanganyifu, ili wawapotoshe wengine kwa hila.

4:15 Ila, sisi tukisema ukweli kwa moyo wa mapendo tutakua zidi katika kila jambo kulingana na Kristo ambaye ndiye kichwa;

4:16 chini ya uongozi wake, viungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo vyake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo, mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.

4:17 Basi, kwa jina la Bwana, nawaonyeni: msiishi tena kama watu wasiomjua Mungu, ambao fikira zao zimekuwa upuuzi mtupu,

4:18 na akili zao zimo gizani. Wako mbali na uzima wa Mungu, kwa sababu ya upumbavu ulio ndani yao na ukaidi wao.

4:19 Wamepotoka na hawana aibu, wamejitosa katika ufisadi; hufanya kwa pupa kila aina ya mambo ya aibu.

4:20 Lakini ninyi hamkujifunza hivyo juu ya Kristo.

4:21 Ni dhahiri kwamba mlisikia barabara habari zake, na mkiwa wafuasi wake mkafundishwa ukweli ulivyo katika Yesu.

4:22 Basi, acheni mwenendo wenu wa awali, yaani ule utu wenu wa kale uliokuwa unaangamizwa kwa tamaa zake danganyifu.

4:23 Jirekebisheni upya rohoni na katika fikira zenu.

4:24 Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa mfano wa Mungu na ambayo hujionyesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu.

4:25 Kwa hiyo, acheni uongo. Kila mmoja anapaswa kumwambia mwenzake ukweli, maana kila mmoja wetu ni kiungo cha mwili wa Kristo.

4:26 Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima.

4:27 Msimpe Ibilisi nafasi.

4:28 Aliyekuwa akiiba, asiibe tena, bali na aanze kufanya kazi njema kwa mikono yake, apate kuwa na kitu cha kumsaidia mtu aliye maskini.

4:29 Maneno mabaya hata yasisikike kamwe miongoni mwenu; kila mara maneno yenu yawe ya kufaa na ambayo hujenga na kuwasaidia wengine, ili yawaneemeshe wasikilizaji wenu.

4:30 Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba ninyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni.

4:31 Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele, matusi! Achaneni na kila uovu!

4:32 Muwe na moyo mwema na wenye kuhurumiana; kila mmoja na amsamehe mwenzake kama naye Mungu alivyowasamehe ninyi kwa njia ya Kristo.

5:1 Kwa hiyo, mwigeni Mungu, maana ninyi ni watoto wake wapenzi.

5:2 Upendo uongoze maisha yenu, kama vile Kristo alivyotupenda, na kwa ajili yetu akajitoa mwenyewe kama dhabihu yenye harufu nzuri na tambiko impendezayo Mungu.

5:3 Kwa vile ninyi ni watu wa Mungu, basi uasherati, uchafu wowote ule au choyo visitajwe kamwe miongoni mwenu.

5:4 Tena maneno ya aibu, ya upuuzi au ubishi, yote hayo hayafai kwenu; maneno ya kumshukuru Mungu ndiyo yanayofaa.

5:5 Jueni wazi kwamba mwasherati yeyote au mchafu au mfisadi, (ufisadi ni sawa na kuabudu sanamu), au mtu yeyote wa aina hiyo hataambulia chochote katika Utawala wa Kristo na wa Mungu.

5:6 Msikubali kudanganywa na mtu kwa maneno matupu; maana, kwa sababu ya mambo kama hayo ghadhabu ya Mungu huwajia wote wasiomtii.

5:7 Basi, msishirikiane nao.

5:8 Zamani ninyi mlikuwa gizani, lakini sasa ninyi mko katika mwanga kwa kuungana na Bwana. Ishini kama watoto wa mwanga:

5:9 maana matokeo ya mwanga ni wema kamili, uadilifu na ukweli.

5:10 Jaribuni kujua yale yanayompendeza Bwana.

5:11 Msishiriki katika matendo yasiyofaa, ya giza bali yafichueni.

5:12 Mambo yanayotendwa kwa siri ni aibu hata kuyataja.

5:13 Lakini mambo yale yanayotendwa katika mwanga, ukweli wake hudhihirishwa;

5:14 na kila kilichodhihirishwa huwa mwanga. Ndiyo maana Maandiko yasema: "Amka wewe uliyelala, fufuka kutoka wafu, naye Kristo atakuangaza."

5:15 Basi, muwe waangalifu jinsi mnavyoishi: Msiishi kama wapumbavu, bali kama wenye hekima.

5:16 Tumieni vizuri muda mlio nao maana siku hizi ni mbaya.

5:17 Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana.

5:18 Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu.

5:19 Zungumzeni kwa maneno ya Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Bwana nyimbo na zaburi kwa shukrani mioyoni mwenu.

5:20 Mshukuruni Mungu Baba daima kwa ajili ya yote, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

5:21 Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya kumcha Kristo.

5:22 Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana.

5:23 Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake.

5:24 Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote.

5:25 Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake.

5:26 Alifanya hivyo, ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji,

5:27 kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safu kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo.

5:28 Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.

5:29 (Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa,

5:30 maana sisi ni viungo vya mwili wake.)

5:31 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Kwa hiyo, mwanamume atawaacha baba na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja."

5:32 Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake.

5:33 Lakini yanawahusu ninyi pia: kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.

6:1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema.

6:2 "Waheshimu Baba na mama yako," hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani,

6:3 "Upate fanaka na miaka mingi duniani."

6:4 Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.

6:5 Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na tetemeko; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo.

6:6 Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu ninyi ni watumishi wa Kristo.

6:7 Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu.

6:8 Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana.

6:9 Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba ninyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, kwake cheo cha mtu si kitu.

6:10 Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu.

6:11 Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi.

6:12 Maana vita vyenu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu wanaomiliki ulimwengu huu wa giza.

6:13 Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika muweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, muwe bado thabiti.

6:14 Basi, simameni imara! Ukweli uwe kama ukanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani,

6:15 na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu.

6:16 Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu.

6:17 Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu.

6:18 Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu.

6:19 Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Habari Njema kwa uthabiti.

6:20 Mimi ni balozi kwa ajili ya Habari Njema hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo.

6:21 Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu wa Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya.

6:22 Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo.

6:23 Ninawatakieni ninyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.

6:24 Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.


Next: Philippians