Sacred Texts  Bible  World Bible  Index  Next 

Swahili Bible: Matthew

1:1 Yesu Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:

1:2 Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake,

1:3 Yuda alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami,

1:4 Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni,

1:5 Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese,

1:6 naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa mke wa Uria).

1:7 Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa,

1:8 Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia,

1:9 Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia,

1:10 Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia,

1:11 Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.

1:12 Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerobabeli,

1:13 Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori,

1:14 Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi,

1:15 Eliudi alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo,

1:16 Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

1:17 Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.

1:18 Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

1:19 Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri.

1:20 Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

1:21 Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao."

1:22 Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii:

1:23 "Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli" (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi").

1:24 Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani.

1:25 Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.

2:1 Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu, mkoani Yudea, wakati Herode alipokuwa mfalme. Punde tu baada ya kuzaliwa kwake, wataalamu wa nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu,

2:2 wakauliza, "Yuko wapi mtoto, Mfalme wa Wayahudi, aliyezaliwa? Tumeiona nyota yake ilipotokea mashariki, tukaja kumwabudu."

2:3 Mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, yeye pamoja na wakazi wote wa Yerusalemu.

2:4 Basi akawaita pamoja makuhani wakuu wote na walimu wa Sheria, akawauliza, "Kristo atazaliwa wapi?"

2:5 Nao wakamjibu, "Mjini Bethlehemu, mkoani Yudea. Ndivyo nabii alivyoandika:

2:6 Ewe Bethlehemu katika nchi ya Yuda, kwa vyovyote wewe si mdogo kabisa kati ya viongozi wa Yuda; maana kwako atatokea kiongozi atakayewaongoza watu wangu, Israeli."

2:7 Hapo, Herode aliwaita faraghani hao wataalamu wa nyota, akawauliza wakati hasa ile nyota ilipowatokea.

2:8 Kisha akawatuma Bethlehemu akisema, "Nendeni mkachunguze kwa makini habari za mtoto huyo. Mkisha mpata nileteeni habari ili nami niende nikamwabudu."

2:9 Baada ya kumsikiliza mfalme, hao wataalamu wa nyota wakaenda. Kumbe ile nyota waliyokuwa wameiona upande wa mashariki iliwatangulia hata ikaenda kusimama juu ya mahali pale alipokuwa mtoto.

2:10 Walipoiona hiyo nyota, walifurahi mno.

2:11 Basi, wakaingia nyumbani, wakamwona yule mtoto pamoja na Maria mama yake; wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi: dhahabu, ubani na manemane.

2:12 Mungu aliwaonya katika ndoto wasimrudie Herode; hivyo wakarudi makwao kwa njia nyingine.

2:13 Baada ya wale wageni kuondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto, akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapokwambia, maana Herode anakusudia kumwua huyu mtoto."

2:14 Hivyo, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akaondoka usiku, akaenda Misri.

2:15 Akakaa huko mpaka Herode alipokufa. Jambo hilo lilifanyika ili neno alilosema Bwana kwa njia ya nabii litimie: "Nilimwita Mwanangu kutoka Misri."

2:16 Herode alipogundua kwamba wale wataalamu wa nyota walikuwa wamemhadaa, alikasirika sana. Akaamuru watoto wote wa kiume mjini Bethlehemu na kandokando yake wenye umri wa miaka miwili na chini yake wauawe. Alifanya hivyo kufuatana na muda aliopata kujua kutoka kwa wale wataalamu wa nyota.

2:17 Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyosemwa kwa njia ya nabii Yeremia:

2:18 "Sauti imesikika mjini Rama, kilio na maombolezo mengi. Raheli anawalilia watoto wake, wala hataki kutulizwa, maana wote wamefariki."

2:19 Baada ya kifo cha Herode, malaika wa Bwana alimtokea Yosefu katika ndoto kule Misri,

2:20 akamwambia, "Amka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake, urudi tena katika nchi ya Israeli, maana wale waliotaka kumwua mtoto huyo wamekwisha kufa."

2:21 Basi, Yosefu aliamka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, akarejea katika nchi ya Israeli.

2:22 Lakini Yosefu aliposikia kwamba Arkelao mwanawe Herode alikuwa mfalme wa Yudea mahali pa baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye baada ya kuonywa katika ndoto, alikwenda katika mkoa wa Galilaya,

2:23 akahamia katika mji uitwao Nazareti. Ndivyo yalivyotimia maneno yaliyonenwa kwa njia ya manabii: "Ataitwa Mnazare."

3:1 Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri katika jangwa la Yudea:

3:2 "Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia."

3:3 Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni vijia vyake."

3:4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.

3:5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,

3:6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.

3:7 Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?

3:8 Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli.

3:9 Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, Baba yetu ni Abrahamu! Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto wa Abrahamu.

3:10 Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo, kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni.

3:11 Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu. Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

3:12 Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto usiozimika."

3:13 Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye.

3:14 Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe."

3:15 Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa, maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo Yohane akakubali.

3:16 Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua juu yake.

3:17 Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu mpendwa, nimependezwa naye."

4:1 Kisha Roho alimwongoza Yesu mpaka jangwani ili ajaribiwe na Ibilisi.

4:2 Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa.

4:3 Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate."

4:4 Yesu akamjibu, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Binadamu hataishi kwa mikate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu."

4:5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu,

4:6 akamwambia, "Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe."

4:7 Yesu akamwambia, "Imeandikwa pia: Usimjaribu Bwana, Mungu wako."

4:8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari zake,

4:9 akamwambia, "Hivi vyote nitakupa kama tu ukipiga magoti na kuniabudu."

4:10 Hapo, Yesu akamwambia, "Nenda zako Shetani! Imeandikwa: Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake."

4:11 Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia.

4:12 Yesu aliposikia kwamba Yohane ametiwa gerezani alikwenda Galilaya.

4:13 Aliondoka Nazareti, akaenda Kafarnaumu, mji ulio kando ya bahari ya Genesareti, mpakani mwa wilaya za Zabuloni na Naftali, akakaa huko.

4:14 Ndivyo lilivyotimia lile neno lililosemwa kwa njia ya nabii Isaya:

4:15 "Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kuelekea baharini ng'ambo ya mto Yordani, Galilaya nchi ya watu wa Mataifa!

4:16 Watu waliokaa gizani wameona mwanga mkubwa. Nao walioishi katika nchi ya giza na kivuli cha kifo, mwanga umewaangazia!"

4:17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, "Tubuni, maana ufalme wa mbinguni umekaribia!"

4:18 Yesu alipokuwa anatembea kando ya ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili wavuvi; Simoni (aitwae Petro) na Andrea, ndugu yake; walikuwa wakivua samaki kwa nyavu ziwani.

4:19 Basi, akawaambia, "Nifuateni, nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."

4:20 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

4:21 Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona ndugu wengine wawili: Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Hao walikuwa ndani ya mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakitengeneza nyavu zao. Basi Yesu akawaita,

4:22 nao mara wakaiacha mashua pamoja na baba yao, wakamfuata.

4:23 Yesu alikuwa anakwenda kila mahali wilayani Galilaya, akifundisha katika masunagogi na kuhubiri Habari Njema juu ya ufalme wa Mungu. Aliponya kila namna ya maradhi na magonjwa waliyokuwa nayo watu.

4:24 Habari zake zikaenea katika mkoa wote wa Siria. Wagonjwa wote wenye maradhi ya kila namna na wale waliosumbuliwa na kila namna ya taabu: waliopagawa na pepo, wenye kifafa na watu waliokuwa wamelemaa, walipelekwa kwake; naye akawaponya wote.

4:25 Makundi mengi ya watu kutoka Galilaya, Dekapoli, Yerusalemu, Yudea na ng'ambo ya mto Yordani, walimfuata.

5:1 Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea,

5:2 naye akaanza kuwafundisha:

5:3 "Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

5:4 Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.

5:5 Heri walio wapole, maana watairithi nchi.

5:6 Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa.

5:7 Heri walio na huruma, maana watahurumiwa.

5:8 Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu.

5:9 Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu.

5:10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao.

5:11 "Heri yenu ninyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu.

5:12 Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu.

5:13 "Ninyi ni chumvi ya dunia! Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu.

5:14 "Ninyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika.

5:15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa chungu, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani.

5:16 Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni."

5:17 "Msidhani ya kuwa nimekuja kutangua Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha.

5:18 Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya Sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia.

5:19 Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika Ufalme wa mbiguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika Ufalme wa mbinguni.

5:20 Ndiyo maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa Mafarisayo na walimu wa Sheria, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni.

5:21 "Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.

5:22 Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: Pumbavu atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.

5:23 Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe,

5:24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi ukatoe sadaka yako.

5:25 "Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani, kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani.

5:26 Kweli nakwambia, hutatoka humo mpaka umemaliza kulipa senti ya mwisho.

5:27 "Mmesikia ya kuwa watu waliambiwa: Usizini!

5:28 Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake.

5:29 Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, ling'oe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu.

5:30 Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali zaidi kupoteza kiungo kimoja cha mwili, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.

5:31 "Ilikwisha semwa pia: Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka.

5:32 Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mtu akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.

5:33 "Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.

5:34 Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu;

5:35 wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu.

5:36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

5:37 Ukisema, Ndiyo, basi iwe Ndiyo; ukisema Siyo, basi iwe kweli Siyo. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.

5:38 "Mmesikia kwamba ilisemwa: Jicho kwa jicho, jino kwa jino.

5:39 Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili.

5:40 Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako.

5:41 Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili.

5:42 Akuombaye mpe, na mtu akitaka kukukopa kitu usimnyime.

5:43 "Mmesikia kwamba ilisemwa: Mpende jirani yako na kumchukia adui yako.

5:44 Lakini mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi

5:45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu.

5:46 Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda ninyi? Hakuna! Kwa maana hata watoza ushuru hufanya hivyo!

5:47 Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo.

5:48 Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

6:1 "Jihadharini msije mkafanya matendo yenu mema mbele ya watu kusudi mwonekane nao. La sivyo, Baba yenu aliye mbinguni hatawapeni tuzo.

6:2 "Basi, unapomsaidia maskini, usijitangaze. Usifanye kama wanafiki wafanyavyo katika masunagogi na njiani ili watu wawasifu. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao.

6:3 Lakini wewe unapomsaidia maskini, fanya hivyo kwamba hata rafiki yako asijue ufanyalo.

6:4 Toa msaada wako kwa siri, na Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.

6:5 "Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masunagogi na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawaambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao.

6:6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango, kisha umwombe Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika, atakutuza.

6:7 "Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi.

6:8 Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba.

6:9 Basi, hivi ndivyo mnavyopaswa kusali: Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe.

6:10 Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.

6:11 Utupe leo chakula chetu tunachohitaji.

6:12 Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea.

6:13 Usitutie katika majaribu, lakini utuokoe na yule Mwovu. is Baadhi ya makala za zamani zina; Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.

6:14 "Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia.

6:15 Lakini msipowasamehe watu makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

6:16 "Mnapofunga, msiwe na huzuni kama wanafiki. Wao hukunja nyuso zao wapate kuonekana na watu kuwa wanafunga. Nawaambieni hakika, hao wamekwisha pata tuzo lao.

6:17 Wewe lakini unapofunga, paka kichwa chako mafuta, nawa uso wako,

6:18 ili mtu yeyote asijue kwamba unafunga, ila ujulikane tu kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza.

6:19 "Msijiwekee hazina hapa duniani ambako nondo na kutu huharibu, na wezi huingia na kuiba.

6:20 Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuiharibu, wala wezi hawaingii wakaiba.

6:21 Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.

6:22 "Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote utakuwa katika mwanga.

6:23 Lakini ikiwa jicho lako ni bovu, mwili wako wote utakuwa katika giza. Basi, ikiwa mwanga ulioko ndani yako ni giza, basi, hilo ni giza la kutisha mno.

6:24 "Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Maana atamchukia mmoja na kumpenda huyo wa pili; au ataambatana na mmoja na kumdharau huyo mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali pamoja.

6:25 "Ndiyo maana nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula na kinywaji mnavyohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. Je, maisha ni chakula tu au zaidi? Na mwili, je, si zaidi ya mavazi?

6:26 Waangalieni ndege wa mwituni: hawapandi, hawavuni, wala hawana ghala yoyoye. Hata hivyo, Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani kuliko hao?

6:27 Ni nani miongoni mwenu kwa kuwa na wasiwasi sana anaweza kuuongeza muda wa maisha yake?

6:28 "Na kuhusu mavazi, ya nini kuwa na wasiwasi? Tazameni maua ya porini jinsi yanavyostawi. Hayafanyi kazi wala hayasokoti.

6:29 Lakini nawaambieni, hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.

6:30 Ikiwa basi Mungu hulivika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatafanya zaidi kwenu ninyi? Enyi watu wenye imani haba!

6:31 "Basi, msiwe na wasiwasi: Tutakula nini, tutakunywa nini, tutavaa nini!

6:32 Maana hayo yote yanahangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo vyote.

6:33 Bali, zingatieni kwanza Ufalme wa Mungu na matakwa yake, na hayo mengine yote mtapewa kwa ziada.

6:34 Basi, msiwe na wasiwasi juu ya kesho; kesho inayo yake. Matatizo ya siku moja yanawatosheni kwa siku hiyo.

7:1 "Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;

7:2 kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.

7:3 Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?

7:4 Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?

7:5 Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.

7:6 "Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.

7:7 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

7:8 Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.

7:9 Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?

7:10 Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?

7:11 Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.

7:12 "Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.

7:13 "Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.

7:14 Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.

7:15 "Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.

7:16 Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!

7:17 Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.

7:18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema.

7:19 Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni.

7:20 Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.

7:21 "Si kila aniambiaye, Bwana, Bwana, ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

7:22 Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.

7:23 Hapo nitawaambia: Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.

7:24 "Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.

7:25 Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.

7:26 "Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.

7:27 Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa."

7:28 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.

7:29 Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.

8:1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata.

8:2 Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia akisema, "Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!"

8:3 Yesu akanyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka! Takasika." Mara huyo mtu akapona ukoma wake.

8:4 Kisha Yesu akamwambia, "Sikiliza, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona."

8:5 Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, ofisa mmoja Mroma alimwendea, akamsihi

8:6 akisema, "Mheshimiwa, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana."

8:7 Yesu akamwambia, "Nitakuja kumponya."

8:8 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.

8:9 Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, Nenda! naye huenda; na mwingine, Njoo! naye huja; na mtumishi wangu, Fanya kitu hiki! naye hufanya."

8:10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, "Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli aliye na imani kama hii.

8:11 Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa mbinguni.

8:12 Lakini wale ambao wangalipaswa kuwa katika Ufalme huo watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno."

8:13 Kisha Yesu akamwambia huyo ofisa Mroma, "Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini." Na mtumishi wake akapona saa ileile.

8:14 Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali.

8:15 Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia.

8:16 Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa.

8:17 Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: "Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, ameyachukua magonjwa yetu."

8:18 Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng'ambo ya ziwa.

8:19 Mwalimu mmoja wa Sheria akamwendea, akamwambia, "Mwalimu, mimi nitakufuata kokote uendako."

8:20 Yesu akamjibu, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia."

8:21 Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, "Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu."

8:22 Lakini Yesu akamwambia, "Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao."

8:23 Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye.

8:24 Ghafla, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu alikuwa amelala usingizi.

8:25 Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, "Bwana, tuokoe, tunaangamia!"

8:26 Yesu akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?" Basi, akainuka, akazikemea pepo na mawimbi; kukawa shwari kabisa.

8:27 Watu wakashangaa, wakasema, "Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na mawimbi vinamtii!"

8:28 Yesu alifika katika nchi ya Wagerasi, ng'ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita katika njia hiyo.

8:29 Nao wakaanza kupiga kelele, "Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?"

8:30 Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa.

8:31 Basi, hao pepo wakamsihi, "Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale."

8:32 Yesu akawaambia, "Haya, nendeni." Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa maji.

8:33 Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa.

8:34 Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.

9:1 Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake.

9:2 Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako."

9:3 Baadhi ya walimu wa Sheria wakaanza kufikiri, "Mtu huyu anamkufuru Mungu!"

9:4 Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, "Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu?

9:5 Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Simama, utembee?

9:6 Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako."

9:7 Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake.

9:8 Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo.

9:9 Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, "Nifuate." Naye Mathayo akainuka, akamfuata.

9:10 Yesu alipokuwa nyumbani ameketi kula chakula, watoza ushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake.

9:11 Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, "Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"

9:12 Yesu aliwasikia, akasema, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi.

9:13 Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: Nataka huruma, wala si dhabihu. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi."

9:14 Kisha wanafunzi wa Yohane mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, "Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?"

9:15 Yesu akawajibu, "Je, walioalikwa arusini wanaweza kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.

9:16 "Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka.

9:17 Wala hakuna mtu awekaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila divai mpya hutiwa katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama."

9:18 Yesu alipokuwa akisema hayo, ofisa mmoja Myahudi alifika, akamwinamia na kusema, "Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini, tafadhali njoo umwekee mkono wako naye ataishi."

9:19 Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake, akamfuata.

9:20 Mama mmoja, mgonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake.

9:21 Alifanya hivyo kwani alifikiri moyoni: "Nikigusa tu vazi lake, nitapona."

9:22 Basi, Yesu akageuka akamwona, akamwambia, "Binti, jipe moyo! Imani yako imekuponya." Mama huyo akapona saa ileile.

9:23 Kisha Yesu akaingia nyumbani kwa yule ofisa. Na alipowaona wapiga filimbi na umati wa watu wanaofanya matanga,

9:24 akasema, "Ondokeni hapa! Msichana huyu hakufa, amelala tu." Nao wakamcheka.

9:25 Basi, umati wa watu ulipoondolewa, Yesu aliingia ndani, akamshika huyo msichana mkono, naye akasimama.

9:26 Habari hiyo ikavuma sana katika nchi ile yote.

9:27 Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda, vipofu wawili walimfuata wakipiga kelele, "Mwana wa Daudi, utuhurumie!"

9:28 Yesu alipoingia nyumbani, vipofu hao wawili wakamwendea, naye akawauliza, "Je, mnaamini kwamba naweza kuwafanyia jambo hilo?" Nao wakamjibu, "Naam, Mheshimiwa."

9:29 Hapo Yesu akayagusa macho yao, akasema, "Na iwe kwenu kama mnavyoamini."

9:30 Macho yao yakafunguliwa. Naye Yesu akawaonya kwa ukali: "Msimwambie mtu yeyote jambo hili."

9:31 Lakini wao wakaondoka, wakaeneza habari za Yesu katika nchi ile yote.

9:32 Watu walipokuwa wanakwenda zao, wengine walimletea Yesu mtu mmoja aliyekuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo.

9:33 Mara tu huyo pepo alipotolewa, mtu huyo aliyekuwa bubu akaanza kuongea tena. Watu wakashangaa na kusema, "Jambo kama hili halijapata kuonekana katika Israeli!"

9:34 Lakini Mafarisayo wakawa wanasema, "Anawatoa pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo wabaya."

9:35 Yesu alitembelea miji yote na vijiji, akafundisha katika masunagogi yao akihubiri Habari Njema ya Ufalme wa Mungu, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila namna.

9:36 Basi, alipowaona watu, makundi kwa makundi, aliwaonea huruma kwa sababu walikuwa hoi na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji.

9:37 Hapo akawaambia wanafunzi wake, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache.

9:38 Kwa hivyo mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake."

10:1 Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote.

10:2 Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake;

10:3 Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;

10:4 Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

10:5 Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: "Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa Wasamaria.

10:6 Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo.

10:7 Mnapokwenda hubirini hivi: Ufalme wa mbinguni umekaribia.

10:8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure.

10:9 Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba.

10:10 Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake.

10:11 "Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka mahali hapo.

10:12 Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake.

10:13 Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu itawarudia ninyi.

10:14 Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung'uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.

10:15 Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.

10:16 "Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa.

10:17 Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao.

10:18 Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa.

10:19 Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema.

10:20 Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

10:21 "Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.

10:22 Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa.

10:23 "Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.

10:24 "Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumishi si mkuu kuliko bwana wake.

10:25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?

10:26 "Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa.

10:27 Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong'onezwa, litangazeni hadharani.

10:28 Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu.

10:29 Shomoro wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu.

10:30 Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

10:31 Kwa hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi.

10:32 "Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

10:33 Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

10:34 "Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga.

10:35 Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake.

10:36 Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.

10:37 "Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

10:38 Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili.

10:39 Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.

10:40 "Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma.

10:41 Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema.

10:42 Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake."

11:1 Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

11:2 Yohane mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake,

11:3 wamwulize: "Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?"

11:4 Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona:

11:5 vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema.

11:6 Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami."

11:7 Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: "Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo?

11:8 Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumtazama mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme.

11:9 Basi, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii.

11:10 "Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: Tazama, hapa namtuma mjumbe wangu, asema Bwana, akutangulie na kukutayarishia njia yako.

11:11 Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye.

11:12 Tangu wakati wa Yohane mbatizaji mpaka leo hii, Ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu.

11:13 Mafundisho yote ya manabii na sheria yalibashiri juu ya nyakati hizi.

11:14 Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Eliya ambaye angekuja.

11:15 Mwenye masikio na asikie!

11:16 "Basi, nitakifananisha kizazi hiki na kitu gani? Ni kama vijana waliokuwa wamekaa uwanjani, wakawa wakiambiana kikundi kimoja kwa kingine:

11:17 Tumewapigieni ngoma lakini hamkucheza; tumeimba nyimbo za huzuni lakini hamkulia!

11:18 Kwa maana Yohane alikuja, akafunga na wala hakunywa divai, nao wakasema: Amepagawa na pepo.

11:19 Mwana wa Mtu akaja, anakula na kunywa, nao wakasema: Mtazameni huyu, mlafi na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wahalifu! Hata hivyo, hekima ya Mungu inathibitishwa kuwa njema kutokana na matendo yake."

11:20 Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kubadili nia zao mbaya:

11:21 "Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia na kujipaka majivu zamani, ili kuonyesha kwamba wametubu.

11:22 Hata hivyo nawaambieni, Siku ya hukumu, ninyi mtapata adhabu kubwa kuliko Tiro na Sidoni.

11:23 Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka Kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo.

11:24 Lakini nawaambieni, Siku ya hukumu itakuwa nafuu zaidi kwa watu wa Sodoma, kuliko kwako wewe."

11:25 Wakati huo Yesu alisema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima mambo haya, ukawafumbulia watoto wadogo.

11:26 Naam Baba, ndivyo ilivyokupendeza.

11:27 "Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana atapenda kumjulisha.

11:28 Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

11:29 Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.

11:30 Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi."

12:1 Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake.

12:2 Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, "Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato."

12:3 Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?

12:4 Yeye aliingia katika Nyumba ya Mungu pamoja na wenzake, wakala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao.

12:5 Au je, hamjasoma katika Sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja Sheria Hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia?

12:6 Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko Hekalu.

12:7 Kama tu mngejua maana ya maneno haya: Nataka huruma wala si dhabihu, hamngewahukumu watu wasio na hatia.

12:8 Maana Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato."

12:9 Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao.

12:10 Kulikuwa na mtu mmoja mwenye mkono uliopooza. Basi, watu wakamwuliza Yesu, "Je, ni halali kumponya mtu siku ya Sabato?" Walimwuliza hivyo wapate kisa cha kumshtaki.

12:11 Lakini Yesu akawaambia, "Tuseme mmoja wenu ana kondoo wake ambaye ametumbukia shimoni; je, hatamshika na kumtoa humo siku ya Sabato?

12:12 Mtu ana thamani kuliko kondoo! Basi, ni halali kutenda mema siku ya Sabato."

12:13 Kisha akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, nao ukawa mzima kabisa kama ule mwingine.

12:14 Basi, Mafarisayo wakatoka nje, wakashauriana jinsi watakavyomwangamiza Yesu.

12:15 Lakini Yesu alipojua jambo hilo, akatoka mahali pale. Watu wengi walimfuata, akawaponya wagonjwa wote,

12:16 akawaamuru wasiwaambie watu habari zake,

12:17 ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie:

12:18 "Hapa ni mtumishi wangu niliyemteua, mpendwa wangu anipendezaye moyoni. Nitaiweka Roho yangu juu yake, naye atatangaza hukumu yangu kwa mataifa yote.

12:19 Hatakuwa na ubishi wala kupiga kelele, wala sauti yake haitasikika barabarani.

12:20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi ufukao moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya hukumu ya haki itawale.

12:21 Katika jina lake mataifa yatakuwa na tumaini."

12:22 Hapo watu wakamletea Yesu kipofu mmoja ambaye alikuwa bubu kwa sababu alikuwa amepagawa na pepo. Yesu akamponya hata, akaweza kusema na kuona.

12:23 Umati wote wa watu ulishangaa ukasema, "Je, huenda ikawa huyu ndiye Mwana wa Daudi?"

12:24 Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, wakasema, "Mtu huyu anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo."

12:25 Yesu, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, "Ufalme wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka.

12:26 Ikiwa Shetani anamfukuza Shetani, anajipinga mwenyewe. Basi, ufalme wake utasimamaje?

12:27 Ninyi mnasema ati nawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli; je, watoto wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo wao ndio watakaowahukumu ninyi.

12:28 Lakini ikiwa ninawafukuza pepo kwa nguvu ya Roho wa Mungu, basi jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu.

12:29 "Au, anawezaje mtu kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang'anya mali yake, bila kwanza kumfunga huyo mtu mwenye nguvu? Hapo ndipo atakapoweza kumnyang'anya mali yake.

12:30 "Yeyote asiyejiunga nami, anapingana nami; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.

12:31 Kwa sababu hiyo, nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.

12:32 Tena, asemaye neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa, lakini yule asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu, hatasamehewa, wala katika ulimwengu huu, wala katika ulimwengu ujao.

12:33 "Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake yatakuwa mema; ufanyeni kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya. Mti hujulikana kwa matunda yake.

12:34 Enyi kizazi cha nyoka! Mnawezaje kusema mambo mema hali ninyi ni waovu? Maana mtu husema kutokana na yale yaliyojaa moyoni.

12:35 Mtu mwema hutoa mambo mema katika hazina yake njema; na mtu mbaya hutoa mambo mabaya katika hazina yake mbaya.

12:36 "Basi, nawaambieni, Siku ya hukumu watu watapaswa kujibu juu ya kila neno lisilofaa wanalosema.

12:37 Maana kwa maneno yako, utakubaliwa kuwa mwadilifu, na kwa maneno yako, utahukumiwa kuwa na hatia."

12:38 Kisha baadhi ya walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamwambia Yesu, "Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako."

12:39 Naye akawajibu, "Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara; hamtapewa ishara nyingine, ila tu ile ishara ya nabii Yona.

12:40 Jinsi Yona alivyokaa siku tatu kutwa kucha tumboni mwa nyangumi, ndivyo naye Mwana wa Mtu atakavyokaa ndani ya ardhi siku tatu kutwa kucha.

12:41 Watu wa Ninewi watatokea siku ya hukumu, nao watakihukumu kizazi hiki kwamba kina hatia. Maana Waninewi walitubu kwa sababu ya mahubiri ya Yona, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Yona!

12:42 Malkia wa kusini atatokea wakati kizazi hiki kitakapohukumiwa, naye atakihukumu kwamba kina hatia. Maana yeye alisafiri kutoka mbali akaja kusikiliza maneno ya hekima ya Solomoni, na kumbe hapa kuna kikuu kuliko Solomoni.

12:43 "Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani akitafuta mahali pa kupumzika asipate.

12:44 Hapo hujisemea: Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka. Lakini anaporudi na kuikuta tupu, imefagiwa na kupambwa,

12:45 huenda kuwachukua pepo wengine saba, wabaya kuliko yeye; na wote huja wakamwingia huyo mtu. Na hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya kuliko hapo mwanzo. Ndivyo itakavyokuwa kwa watu hawa waovu."

12:46 Yesu alikuwa bado anasema na umati wa watu wakati mama yake na ndugu zake walipofika na kusimama nje, wakitaka kusema naye.

12:47 Basi, mtu mmoja akamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kusema nawe."

12:48 Lakini Yesu akamjibu mtu huyo, "Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni kina nani?"

12:49 Kisha akaunyosha mkono wake kuelekea wanafunzi wake, akasema, "Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu!

12:50 Maana yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu."

13:1 Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa.

13:2 Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashua, akaketi. Hao watu walisimama kwenye ukingo wa ziwa,

13:3 naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.

13:4 Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.

13:5 Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.

13:6 Jua lilipochomoza, zilichomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.

13:7 Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga.

13:8 Lakini nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: nyingine punje mia moja, nyingine sitini na nyingine thelathini.

13:9 Mwenye masikio na asikie!"

13:10 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, "Kwa nini unasema na watu kwa mifano?"

13:11 Yesu akawajibu, "Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.

13:12 Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

13:13 Ndiyo maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.

13:14 Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

13:15 Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao. wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.

13:16 "Lakini heri yenu ninyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia.

13:17 Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.

13:18 "Basi, ninyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi.

13:19 Yeyote asikiaye ujumbe wa ufalme bila kuuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake.

13:20 Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye ujumbe huo na mara akaupokea kwa furaha.

13:21 Lakini haumwingii na kuwa na mizizi ndani yake; huendelea kuuzingatia ujumbe huo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya ujumbe huo, anakata tamaa mara.

13:22 Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye huo ujumbe, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali huusonga ujumbe huo, naye hazai matunda.

13:23 Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu ausikiaye ujumbe huo na kuuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini."

13:24 Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.

13:25 Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.

13:26 Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.

13:27 Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, Mheshimiwa, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?

13:28 Yeye akawajibu, Adui ndiye aliyefanya hivyo. Basi, watumishi wake wakamwuliza, Je, unataka twende tukayang'oe

13:29 Naye akawajibu, La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang'oa na ngano pia.

13:30 Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu."

13:31 Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.

13:32 Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikishaota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, na ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake."

13:33 Yesu akawaambia mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga pishi tatu, hata unga wote ukaumuka."

13:34 Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano,

13:35 ili jambo lililonenwa na nabii litimie: "Nitasema kwa mifano; nitawaambia mambo yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu."

13:36 Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani."

13:37 Yesu akawaambia, "Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu.

13:38 Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao Ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.

13:39 Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika.

13:40 Kama vile magugu yanavyokusanywa kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;

13:41 Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika Ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu,

13:42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, na huko watalia na kusaga meno.

13:43 Kisha, wale wema watang'ara kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Sikieni basi, kama mna masikio!

13:44 "Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.

13:45 "Tena, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri.

13:46 Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.

13:47 "Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina.

13:48 Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.

13:49 Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema,

13:50 na kuwatupa hao wabaya katika tanuru ya moto. Huko watalia na kusaga meno."

13:51 Yesu akawauliza, "Je, mmeelewa mambo haya yote?" Wakamjibu, "Naam."

13:52 Naye akawaambia, "Hivyo basi, kila mwalimu wa Sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale."

13:53 Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo,

13:54 akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi hata wakashangaa, wakasema, "Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu?

13:55 Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?

13:56 Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?"

13:57 Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, "Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!"

13:58 Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.

14:1 Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu.

14:2 Basi, akawaambia watumishi wake, "Mtu huyu ni Yohane mbatizaji, amefufuka kutoka wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake."

14:3 Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Sababu hasa ni

14:4 kwamba alikuwa amemwambia Herode, "Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!"

14:5 Herode alitaka kumwua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii.

14:6 Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa,

14:7 hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba.

14:8 Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, "Nipe papahapa katika sinia kichwa cha Yohane mbatizaji."

14:9 Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe.

14:10 Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane.

14:11 Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake.

14:12 Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.

14:13 Yesu alipopata habari hiyo, aliondoka mahali pale kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake. Lakini watu walipata habari, wakamfuata kwa miguu toka mijini.

14:14 Basi, aliposhuka pwani, aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, akawaponya wagonjwa wao.

14:15 Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea wakamwambia, "Mahali hapa ni nyikani, na saa zimepita. Basi, uwaage watu ili waende vijijini wakajinunulie chakula."

14:16 Yesu akawaambia, "Si lazima waende, wapeni ninyi chakula."

14:17 Lakini wao wakamwambia, "Tunayo mikate mitano tu na samaki wawili."

14:18 Yesu akawaambia, "Nileteeni hapa."

14:19 Akawaamuru watu waketi katika nyasi. Kisha akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akamshukuru Mungu. Halafu akaimega hiyo mikate, akawapa wanafunzi wake, nao wakawapa watu.

14:20 Watu wote wakala, wakashiba. Kisha wanafunzi wakakusanya mabaki, wakajaza vikapu kumi na viwili.

14:21 Jumla ya waliokula ilikuwa wanaume wapatao elfu tano, bila kuhesabu wanawake na watoto.

14:22 Mara, Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie ng'ambo ya ziwa wakati yeye anawaaga watu.

14:23 Baada ya kuwaaga, alipanda mlimani peke yake kusali. Ilipokuwa jioni, yeye alikuwa huko peke yake,

14:24 na wakati huo ile mashua ilikwishafika karibu katikati ya ziwa, lakini ilikuwa inakwenda mrama kwa sababu upepo ulikuwa unaipinga.

14:25 Usiku, karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji.

14:26 Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji waliingiwa na hofu, wakasema, "Ni mzimu!" Wakapiga kelele kwa hofu.

14:27 Mara, Yesu akasema nao, "Tulieni, ni mimi. Msiogope!"

14:28 Petro akamwambia, "Bwana, ikiwa ni wewe kweli, amuru nitembee juu ya maji nije kwako."

14:29 Yesu akasema, "Haya, njoo." Basi, Petro akashuka kutoka ile mashua, akatembea juu ya maji, akamwendea Yesu.

14:30 Lakini alipouona ule upepo, aliogopa, akaanza kuzama; akalia kwa sauti, "Bwana, niokoe!"

14:31 Hapo, Yesu akaunyosha mkono wake, akamshika na kumwambia, "Ewe mwenye imani haba! Kwa nini uliona shaka?"

14:32 Basi, wakapanda mashuani, na upepo ukatulia.

14:33 Wote waliokuwa ndani ya mashua walimsujudia, wakasema, "Hakika wewe ni Mwana wa Mungu."

14:34 Walivuka ziwa, wakafika nchi ya Genesareti.

14:35 Watu wa huko walipomtambua, wakaeneza habari pote katika sehemu hizo. Basi, wakamletea Yesu wagonjwa wote,

14:36 wakamwomba awaruhusu waguse tu pindo la vazi lake; wote waliomgusa walipona.

15:1 Kisha Mafarisayo na walimu wa Sheria wakafika kutoka Yerusalemu, wakamwendea Yesu, wakamwuliza,

15:2 "Kwa nini wanafunzi wako hawajali mapokeo tuliyopokea kutoka kwa wazee wetu? Hawanawi mikono yao kama ipasavyo kabla ya kula!"

15:3 Yesu akawajibu, "Kwa nini nanyi mnapendelea mapokeo yenu wenyewe na hamuijali Sheria ya Mungu?

15:4 Mungu amesema: Waheshimu baba yako na mama yako, na Anayemkashifu baba yake au mama yake, lazima auawe.

15:5 Lakini ninyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema: Kitu hiki nimemtolea Mungu,

15:6 basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.

15:7 Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:

15:8 Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno tu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

15:9 Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu."

15:10 Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, "Sikilizeni na muelewe!

15:11 Kitu kinachomtia mtu najisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu najisi."

15:12 Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, "Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?"

15:13 Lakini yeye akawajibu, "Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakuupanda, utang'olewa.

15:14 Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni."

15:15 Petro akadakia, "Tufafanulie huo mfano."

15:16 Yesu akasema, "Hata nyinyi hamwelewi?

15:17 Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutupwa nje chooni?

15:18 Lakini yale yatokayo kinywani hutoka moyoni, na hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi.

15:19 Maana moyoni hutoka mawazo maovu yanayosababisha uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na kashfa.

15:20 Hayo ndiyo yanayomtia mtu najisi. Lakini kula chakula bila kunawa mikono hakumtii mtu najisi."

15:21 Yesu aliondoka mahali hapo akaenda kukaa katika sehemu za Tiro na Sidoni.

15:22 Basi, mama mmoja Mkaanani wa nchi hiyo alimjia, akapaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, nionee huruma! Binti yangu anasumbuliwa na pepo."

15:23 Lakini Yesu hakumjibu neno. Basi, wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Mwambie aende zake kwa maana anatufuatafuata akipiga kelele."

15:24 Yesu akajibu, "Sikutumwa ila kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo."

15:25 Hapo huyo mama akaja, akapiga magoti mbele yake, akasema, "Mheshimiwa, nisaidie."

15:26 Yesu akamjibu, "Si sawa kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa."

15:27 Huyo mama akajibu, "Ni kweli, Mheshimiwa; lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka meza ya bwana wao."

15:28 Hapo Yesu akamjibu, "Mama, imani yako ni kubwa; basi, ufanyiwe kama unavyotaka." Yule binti yake akapona tangu saa hiyo wakati huohuo.

15:29 Yesu alitoka hapo akaenda kando ya ziwa Galilaya, akapanda mlimani, akaketi.

15:30 Watu wengi sana wakamjia wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi waliokuwa wagonjwa, wakawaweka mbele ya miguu yake, naye Yesu akawaponya.

15:31 Umati ule wa watu ulishangaa sana ulipoona bubu wakiongea, waliokuwa wamelemaa wamepona, viwete wakitembea na vipofu wakiona; wakamsifu Mungu wa Israeli.

15:32 Basi, Yesu aliwaita wanafunzi wake, akasema, "Nawaonea watu hawa huruma kwa sababu kwa siku tatu wamekuwa nami, wala hawana chakula. Sipendi kuwaacha waende bila kula wasije wakazimia njiani."

15:33 Wanafunzi wakamwambia, "Hapa tuko nyikani; tutapata wapi chakula cha kuwatosha watu wengi hivi?"

15:34 Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Wakamjibu, "Saba na visamaki vichache."

15:35 Basi, Yesu akawaamuru watu wakae chini.

15:36 Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akamshukuru Mungu, akavimega, akawapa wanafunzi, nao wakawagawia watu.

15:37 Wote wakala, wakashiba. Kisha wakakusanya makombo, wakajaza vikapu saba.

15:38 Hao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila kuhesabu wanawake na watoto.

15:39 Basi, Yesu akawaaga watu, akapanda mashua, akaenda katika eneo la Magadani.

16:1 Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye ishara itokayo mbinguni.

16:2 Lakini Yesu akawajibu, "Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!

16:3 Na alfajiri mwasema: Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda! Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.

16:4 Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote isipokuwa tu ile ya Yona." Basi, akawaacha, akaenda zake.

16:5 Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate.

16:6 Yesu akawaambia, "Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!"

16:7 Lakini wao wakawa wanajadiliana: "Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate."

16:8 Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?

16:9 Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo?

16:10 Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?

16:11 Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!"

16:12 Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

16:13 Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?"

16:14 Wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii."

16:15 Yesu akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?"

16:16 Simoni Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai."

16:17 Yesu akasema, "Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni.

16:18 Nami nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda.

16:19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni."

16:20 Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.

16:21 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: "Ni lazima mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu nitafufuliwa."

16:22 Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: "Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!"

16:23 Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, "Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!"

16:24 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

16:25 Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza;

16:26 lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?

16:27 Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

16:28 Kweli nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika Ufalme wake."

17:1 Baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohane nduguye, akaenda nao peke yao juu ya mlima mrefu.

17:2 Huko, wakiwa wanamtazama, akageuka sura, uso wake ukang'aa kama jua na mavazi yake yakawa meupe kama nuru.

17:3 Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza naye.

17:4 Hapo Petro akamwambia Yesu, "Bwana, ni vizuri sana kwamba tupo hapa! Ukipenda nitajenga vibanda vitatu: kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Eliya."

17:5 Alipokuwa bado anasema hivyo, wingu jeupe likawafunika, na sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: "Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye, msikilizeni."

17:6 Wanafunzi waliposikia hivyo wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana.

17:7 Yesu akawaendea, akawagusa, akasema, "Simameni, msiogope!"

17:8 Walipoinua macho yao hawakumwona mtu, ila Yesu peke yake.

17:9 Basi, walipokuwa wanashuka mlimani, Yesu akawaonya: "Msimwambie mtu mambo mliyoyaona mpaka Mwana wa Mtu atakapofufuliwa kutoka wafu."

17:10 Kisha wanafunzi wakamwuliza, "Mbona walimu wa Sheria wanasema ati ni lazima kwanza Eliya aje?"

17:11 Yesu akawajibu, "Kweli, Eliya atakuja kutayarisha mambo yote.

17:12 Lakini nawaambieni, Eliya amekwisha kuja nao hawakumtambua, bali walimtendea jinsi walivyotaka. Mwana wa Mtu atateswa vivyo hivyo mikononi mwao."

17:13 Hapo hao wanafunzi wakafahamu kwamba alikuwa akiwaambia juu ya Yohane mbatizaji.

17:14 Walipojiunga tena na ule umati wa watu, mtu mmoja alimwendea Yesu, akampigia magoti,

17:15 akasema, "Mheshimiwa, mwonee huruma mwanangu kwa kuwa ana kifafa, tena anateseka sana; mara nyingi yeye huanguka motoni na majini.

17:16 Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya."

17:17 Yesu akajibu, "Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia ninyi mpaka lini? Mleteni hapa huyo mtoto."

17:18 Basi, Yesu akamkemea huyo pepo, naye akamtoka, na yule mtoto akapona wakati huohuo.

17:19 Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha, wakamwuliza, "Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?"

17:20 Yesu akawajibu, "Kwa sababu ya imani yenu haba. Nawaambieni kweli, kama tu mkiwa na imani, hata iwe ndogo kama mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu: Toka hapa uende pale, nao utakwenda. Hakuna chochote ambacho hakingewezekana kwenu."

17:21 "Pepo wa namna hii hawezi kuondolewa ila kwa sala na kufunga."

17:22 Walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu aliwaambia, "Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa watu.

17:23 Watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa." Wanafunzi wakahuzunika mno.

17:24 Walipofika Kafarnaumu watu wenye kukusanya fedha ya zaka ya Hekalu walimwendea Petro, wakamwuliza, "Je, mwalimu wenu hulipa fedha ya zaka?"

17:25 Petro akajibu, "Naam, hulipa." Basi, Petro alipoingia ndani ya nyumba, kabla hata hajasema neno, Yesu akamwuliza, "Simoni, wewe unaonaje? Wafalme wa dunia hukusanya ushuru au kodi kutoka kwa kina nani? Kutoka kwa wananchi ama kutoka kwa wageni?"

17:26 Petro akajibu, "Kutoka kwa wageni." Yesu akamwambia, "Haya basi, wananchi hawahusiki.

17:27 Lakini kusudi tusiwakwaze, nenda ziwani ukatupe ndoana; chukua samaki wa kwanza atakayenaswa, fungua kinywa chake, na ndani utakuta fedha taslimu ya zaka. Ichukue ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako."

18:1 Wakati ule wanafunzi walimwendea Yesu, wakamwuliza, "Ni nani aliye mkuu katika Ufalme wa mbinguni?"

18:2 Yesu akamwita mtoto mmoja, akamsimamisha kati yao,

18:3 kisha akasema, "Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika Ufalme wa mbinguni.

18:4 Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika Ufalme wa mbinguni.

18:5 Yeyote anayemkaribisha mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananikaribisha mimi.

18:6 "Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari.

18:7 Ole wake ulimwengu kwa sababu ya vikwazo vinavyowaangusha wengine. Vikwazo hivyo ni lazima vitokee lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.

18:8 "Kama mkono au mguu wako ukikukosesha, ukate na kuutupa mbali nawe. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima bila mkono au mguu, kuliko kutupwa katika moto wa milele ukiwa na mikono miwili na miguu yako miwili.

18:9 Na kama jicho lako likikukosesha, ling'oe na kulitupa mbali nawe. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa chongo, kuliko kutupwa katika moto wa Jehanamu ukiwa na macho yako yote mawili.

18:10 "Jihadharini! Msimdharau mmojawapo wa wadogo hawa. Nawaambieni, malaika wao huko mbinguni wako daima mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

18:11 Maana Mwana wa Mtu alikuja kuwaokoa wale waliopotea.

18:12 Mnaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, akimpoteza mmoja, hufanyaje? Huwaacha wale tisini na tisa mlimani, na huenda kumtafuta yule aliyepotea.

18:13 Akimpata, nawaambieni kweli, humfurahia huyo kuliko awafurahiavyo wale tisini na tisa ambao hawakupotea.

18:14 Hali kadhalika, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmoja wa hawa wadogo apotee.

18:15 "Ndugu yako akikukosea, mwendee ukamwonye mkiwa ninyi peke yenu. Akikusikia utakuwa umempata ndugu yako.

18:16 Asipokusikia, chukua mtu mmoja au wawili pamoja nawe, ili kwa mawaidha ya mashahidi wawili au watatu, kila tatizo litatuliwe.

18:17 Asipowasikia hao, liambie kanisa. Na kama hatalisikia kanisa, na awe kwako kama watu wasiomjua Mungu na watoza ushuru.

18:18 "Nawaambieni kweli, mtakachofunga duniani kitafungwa mbinguni, na mtakachofungua duniani kitafunguliwa mbinguni.

18:19 Tena nawaambieni, wawili miongoni mwenu wakikubaliana hapa duniani kuhusu jambo lolote la kuomba, Baba yangu wa mbinguni atawafanyia jambo hilo.

18:20 Kwa maana popote pale wanapokusanyika wawili au watatu kwa jina langu, mimi nipo hapo kati yao."

18:21 Kisha Petro akamwendea Yesu, akamwuliza, "Je, ndugu yangu akinikosea, nimsamehe mara ngapi? Mara saba?"

18:22 Yesu akamjibu, "Sisemi mara saba tu, bali sabini mara saba.

18:23 Ndiyo maana Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyeamua kukagua hesabu za watumishi wake.

18:24 Ukaguzi ulipoanza, akaletewa mtu mmoja aliyekuwa na deni la fedha talanta elfu kumi.

18:25 Mtu huyo hakuwa na chochote cha kulipa; hivyo bwana wake aliamuru wauzwe, yeye, mke wake, watoto wake na vitu vyote alivyokuwa navyo, ili deni lilipwe.

18:26 Basi, huyo mtumishi akapiga magoti mbele yake, akasema, Unisubiri nami nitakulipa deni lote.

18:27 Yule bwana alimwonea huruma, akamsamehe lile deni, akamwacha aende zake.

18:28 "Lakini huyo mtumishi akaondoka, akamkuta mmoja wa watumishi wenzake aliyekuwa na deni lake fedha denari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akisema, Lipa deni lako!

18:29 Huyo mtumishi mwenzake akapiga magoti, akamwomba, Unisubiri nami nitalipa deni langu lote.

18:30 Lakini yeye hakutaka, bali alimtia gerezani mpaka hapo atakapolipa lile deni.

18:31 "Basi, watumishi wenzake walipoona jambo hilo walisikitika sana, wakaenda kumpasha habari bwana wao juu ya mambo hayo yaliyotukia.

18:32 Hapo yule bwana alimwita huyo mtumishi, akamwambia, Wewe ni mtumishi mbaya sana! Uliniomba, nami nikakusamehe deni lako lote.

18:33 Je, haikukupasa nawe kumhurumia mtumishi mwenzako kama nilivyokuhurumia?

18:34 "Basi, huyo bwana alikasirika sana, akamtoa huyo mtumishi aadhibiwe mpaka hapo atakapolipa deni lote.

18:35 Na baba yangu aliye mbinguni atawafanyieni vivyo hivyo kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kwa moyo wake wote."

19:1 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda katika mkoa wa Yudea, ng'ambo ya mto Yordani.

19:2 Watu wengi walimfuata huko, naye akawaponya.

19:3 Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, "Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?"

19:4 Yesu akawajibu, "Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke,

19:5 na akasema: Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?

19:6 Kwa hiyo wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe."

19:7 Lakini wao wakamwuliza, "Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?"

19:8 Yesu akawajibu, "Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.

19:9 Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini."

19:10 Wanafunzi wake wakamwambia, "Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa."

19:11 Yesu akawaambia, "Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu.

19:12 Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee."

19:13 Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea.

19:14 Yesu akasema, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana Ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa."

19:15 Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.

19:16 Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, "Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uzima wa milele?"

19:17 Yesu akamwambia, "Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uzima, shika amri."

19:18 Yule mtu akamwuliza, "Amri zipi?" Yesu akasema, "Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo,

19:19 waheshimu baba yako na mama yako; na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."

19:20 Huyo kijana akamwambia, "Hayo yote nimeyazingatia tangu utoto wangu; sasa nifanye nini zaidi?"

19:21 Yesu akamwambia, "Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako uwape maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate."

19:22 Huyo kijana aliposikia hayo, alienda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.

19:23 Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kweli nawaambieni, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.

19:24 Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni."

19:25 Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa, wakamwuliza, "Ni nani basi, awezaye kuokoka?"

19:26 Yesu akawatazama, akasema, "Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana."

19:27 Kisha Petro akasema, "Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?"

19:28 Yesu akawaambia, "Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake katika ulimwengu mpya, ninyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.

19:29 Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uzima wa milele.

19:30 Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

20:1 "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.

20:2 Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.

20:3 Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.

20:4 Akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.

20:5 Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.

20:6 Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?

20:7 Wakamjibu: Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Yeye akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.

20:8 "Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.

20:9 Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja.

20:10 Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.

20:11 Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung'unikia yule bwana.

20:12 Wakasema, Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?

20:13 "Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?

20:14 Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

20:15 Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"

20:16 Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho."

20:17 Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,

20:18 "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe.

20:19 Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa."

20:20 Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.

20:21 Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto."

20:22 Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza."

20:23 Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu."

20:24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.

20:25 Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao.

20:26 Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;

20:27 na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.

20:28 Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."

20:29 Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.

20:30 Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"

20:31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"

20:32 Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka niwafanyie nini?"

20:33 Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe."

20:34 Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.

21:1 Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,

21:2 akawaambia, "Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu.

21:3 Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, Bwana anawahitaji, naye atawaachieni mara."

21:4 Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie:

21:5 "Uambieni mji wa Sioni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwana punda, mtoto wa punda."

21:6 Hivyo, wale wanafunzi walienda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza.

21:7 Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake.

21:8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani.

21:9 Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaaza sauti: "Hosana Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Hosana Mungu juu mbinguni!"

21:10 Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, "Huyu ni nani?"

21:11 Watu katika ule umati wakasema, "Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti katika mkoa wa Galilaya."

21:12 Basi, Yesu akaingia Hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya Hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa.

21:13 Akawaambia, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala. Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi."

21:14 Vipofu na vilema walimwendea huko Hekaluni, naye Yesu akawaponya.

21:15 Basi, makuhani wakuu na walimu wa Sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaaza sauti zao Hekaluni wakisema: "Sifa kwa Mwana wa Daudi," wakakasirika.

21:16 Hivyo wakamwambia, "Je, husikii wanachosema?" Yesu akawajibu, "Naam, nasikia! Je hamjasoma Maandiko haya Matakatifu? Kwa vinywa vya watoto wadogo na wanyonyao unajipatia sifa kamilifu."

21:17 Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.

21:18 Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa.

21:19 Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauma chochote ila majani matupu. Basi akauambia, "Usizae tena matunda milele!" Papo hapo huo mtini ukanyauka.

21:20 Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, "Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?"

21:21 Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: Ng'oka ukajitose baharini, itafanyika hivyo.

21:22 Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata."

21:23 Yesu aliingia Hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, "Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?"

21:24 Yesu akawajibu, "Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.

21:25 Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?" Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: "Tukisema, Yalitoka mbinguni, atatuuliza, Basi, mbona hamkumsadiki?

21:26 Na tukisema, Yalitoka kwa watu, tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii."

21:27 Basi, wakamjibu, "Hatujui!" Naye Yesu akawaambia, "Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.

21:28 "Ninyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.

21:29 Yule kijana akamwambia, Sitaki! Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi.

21:30 Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, Naam baba! Lakini hakwenda kazini.

21:31 Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?" Wakamjibu, "Yule mtoto wa kwanza." Basi, Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, watoza ushuru na waasherati wataingia katika Ufalme wa Mungu kabla yenu.

21:32 Maana Yohane alikuja kwenu akawaonyesha njia njema ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watoza ushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote ninyi hamkubadili mioyo yenu, na hamkusadiki."

21:33 Yesu akasema, "Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda nchi ya mbali.

21:34 Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.

21:35 Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamwua na mwingine wakampiga mawe.

21:36 Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile.

21:37 Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: Watamheshimu mwanangu.

21:38 Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!

21:39 Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamwua.

21:40 "Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?"

21:41 Wao wakamjibu, "Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wa mavuno."

21:42 Hapo Yesu akawaambia, "Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!

21:43 "Kwa hiyo nawaambieni, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake."

21:44 "Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda."

21:45 Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao.

21:46 Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.

22:1 Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano:

22:2 "Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi.

22:3 Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje arusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika.

22:4 Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa: karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ng'ombe wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari, njoni arusini.

22:5 Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake,

22:6 na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua.

22:7 Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao.

22:8 Kisha akawaambia watumishi wake: Karamu ya arusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili.

22:9 Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje arusini.

22:10 Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya arusi ikajaa wageni.

22:11 "Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya arusi.

22:12 Mfalme akamwuliza, Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la arusi? Lakini yeye akakaa kimya.

22:13 Hapo mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno."

22:14 Yesu akamaliza kwa kusema, "Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa."

22:15 Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake.

22:16 Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako.

22:17 Haya, twambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa Kaisari?"

22:18 Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, "Enyi

22:19 Nionyesheni fedha ya kulipia kodi." Nao wakamtolea sarafu ya fedha. sarafu ya fedha.

22:20 Basi, Yesu akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?"

22:21 Wakamjibu, "Ni vya Kaisari." Hapo Yesu akawaambia, "Basi, mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari, na Mungu yaliyo yake Mungu."

22:22 Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.

22:23 Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. Hao ndio wale wasemao kwamba wafu hawafufuki.

22:24 Basi, wakamwambia, "Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, amzalie ndugu yake watoto.

22:25 Sasa, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane.

22:26 Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba.

22:27 Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama.

22:28 Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana Wote saba walimwoa."

22:29 Yesu akawajibu, "Kweli mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu!

22:30 Maana wafu watakapofufuliwa hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika mbinguni.

22:31 Lakini kuhusu suala la wafu kufufuka, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu?

22:32 Aliwaambia, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo! Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai."

22:33 Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.

22:34 Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja.

22:35 Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu,

22:36 "Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika Sheria ya Mose?"

22:37 Yesu akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote.

22:38 Hii ndiyo amri kuu ya kwanza.

22:39 Ya pili inafanana na hiyo: Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.

22:40 Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili."

22:41 Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza,

22:42 "Ninyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?" Wakamjibu, "Wa Daudi."

22:43 Yesu akawaambia, "Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema:

22:44 Bwana alimwambia Bwana wangu: keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.

22:45 Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo Bwana, anawezaje kuwa mwanawe?"

22:46 Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.

23:1 Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake,

23:2 "Walimu wa Sheria na Mafarisayo wana mamlaka ya kufafanua Sheria ya Mose.

23:3 Kwa hiyo shikeni na kutekeleza chochote watakachowaambieni. Lakini msiyaige matendo yao, maana hawatekelezi yale wanayoyahubiri.

23:4 Hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani, lakini wao wenyewe hawataki kunyosha hata kidole wapate kuibeba.

23:5 Wao hufanya matendo yao yote ili watu wawaone. Huvaa tepe zenye maandishi ya Sheria juu ya panda la uso na mikononi na hupanua pindo za makoti yao.

23:6 Hupenda nafasi za heshima katika karamu na viti vya heshima katika masunagogi.

23:7 Hupenda kusalimiwa kwa heshima sokoni na kupendelea kuitwa na watu: Mwalimu.

23:8 Lakini ninyi msiitwe kamwe Mwalimu, maana mwalimu wenu ni mmoja tu, nanyi nyote ni ndugu.

23:9 Wala msimwite mtu yeyote Baba hapa duniani, maana Baba yenu ni mmoja tu aliye mbinguni.

23:10 Wala msiitwe Viongozi, maana kiongozi wenu ni mmoja tu, ndiye Kristo.

23:11 Aliye mkubwa miongoni mwenu ni lazima awe mtumishi wenu.

23:12 Anayejikweza atashushwa, na anayejishusha atakwezwa.

23:13 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnaufunga mlango wa Ufalme wa mbinguni mbele ya macho ya watu. Ninyi wenyewe hamwingii ndani, wala hamwaruhusu wanaotaka kuingia waingie.

23:14 Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnawanyonya wajane na kujisingizia kuwa watu wema kwa kusali sala ndefu. Kwa sababu hiyo mtapata adhabu kali.

23:15 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumpata mtu mmoja afuate dini yenu. Mnapompata, mnamfanya astahili maradufu kwenda katika moto wa Jehanamu kuliko ninyi wenyewe.

23:16 "Ole wenu viongozi vipofu! Ninyi mwasema ati mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, kiapo hicho kinamshika.

23:17 Enyi vipofu wapumbavu! Kipi kilicho cha maana zaidi: dhahabu au Hekalu linalofanya hiyo dhahabu kuwa takatifu?

23:18 Tena mwasema ati mtu akiapa kwa madhabahu si kitu; lakini akiapa kwa zawadi iliyowekwa juu ya madhabahu, kiapo hicho humshika.

23:19 Enyi vipofu! Ni kipi kilicho cha maana zaidi: ile zawadi, au madhabahu ambayo hufanya hiyo zawadi kuwa takatifu?

23:20 Anayeapa kwa madhabahu ameapa kwa hiyo madhabahu, na kwa chochote kilichowekwa juu yake.

23:21 Na anayeapa kwa Hekalu ameapa kwa hilo Hekalu na pia kwa yule akaaye ndani yake.

23:22 Na anayeapa kwa mbingu ameapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa huyo aketiye juu yake.

23:23 Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnatoza watu zaka, hata juu ya majani yenye harufu nzuri, bizari na jira, na huku mnaacha mambo muhimu ya Sheria kama vile haki, huruma na imani. Haya ndiyo hasa mliyopaswa kuyazingatia bila kusahau yale mengine.

23:24 Viongozi vipofu! Mnatoa nzi katika kinywaji, lakini mnameza ngamia!

23:25 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnasafisha kikombe na bakuli kwa nje, lakini ndani mnaacha kumejaa vitu mlivyopata kwa unyang'anyi na uchoyo.

23:26 Mfarisayo kipofu! Kisafishe kikombe ndani kwanza na nje kutakuwa safi pia.

23:27 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mko kama makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanaonekana kuwa mazuri, lakini ndani yamejaa mifupa ya maiti na kila namna ya uchafu.

23:28 Hali kadhalika ninyi mnaonekana na watu kwa nje kuwa wema, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

23:29 "Ole wenu walimu wa Sheria na Mafarisayo, wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya watu wema.

23:30 Mwasema: Kama sisi tungaliishi nyakati za wazee wetu hatungalishirikiana nao katika mauaji ya manabii!

23:31 Hivyo mnathibitisha ninyi wenyewe kwamba ninyi ni watoto wa watu waliowaua manabii.

23:32 Haya, kamilisheni ile kazi wazee wenu waliyoianza!

23:33 Enyi kizazi cha nyoka wenye sumu! Mnawezaje kuiepa hukumu ya moto wa Jehanamu?

23:34 Ndiyo maana mimi ninawapelekea ninyi manabii, watu wenye hekima na walimu; mtawaua na kuwasulubisha baadhi yao, na wengine mtawapiga viboko katika masunagogi yenu na kuwasaka katika kila mji.

23:35 Hivyo lawama yote itawapateni kwa ajili ya damu yote ya watu wema iliyomwagwa juu ya ardhi. Naam, tangu kuuawa kwa Abeli ambaye hakuwa na hatia, mpaka kuuawa kwa Zakariya, mwana wa Barakia, ambaye mlimuua Hekaluni kati ya patakatifu na madhabahu.

23:36 Nawaambieni kweli, kizazi hiki kitapata adhabu kwa sababu ya mambo haya.

23:37 "Yerusalemu, Ee Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako. Mara ngapi nimejaribu kuwakusanya watoto wako kwangu, kama vile kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka.

23:38 Haya basi, nyumba yako itaachwa mahame.

23:39 Nakwambia kweli, hutaniona tena mpaka wakati utakaposema: Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."

24:1 Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu.

24:2 Yesu akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."

24:3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?"

24:4 Yesu akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.

24:5 Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: Mimi ndiye Kristo, nao watawapotosha watu wengi.

24:6 Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.

24:7 Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.

24:8 Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.

24:9 "Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu.

24:10 Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.

24:11 Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.

24:12 Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.

24:13 Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka.

24:14 Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.

24:15 "Basi, mtakapoona Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),

24:16 hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.

24:17 Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.

24:18 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

24:19 Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

24:20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato!

24:21 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.

24:22 Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.

24:23 "Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: Kristo yuko hapa au Yuko pale, msimsadiki.

24:24 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu.

24:25 Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati.

24:26 Basi, wakiwaambieni, Tazameni, yuko jangwani, msiende huko; au, Tazameni, amejificha ndani, msisadiki;

24:27 maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

24:28 Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

24:29 "Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

24:30 Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.

24:31 Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.

24:32 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

24:33 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.

24:34 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

24:35 Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

24:36 "Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye.

24:37 Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

24:38 Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.

24:39 Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.

24:40 Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

24:41 Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

24:42 Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.

24:43 Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.

24:44 Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."

24:45 Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake?

24:46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.

24:47 Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote.

24:48 Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: Bwana wangu anakawia kurudi,

24:49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi,

24:50 bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.

24:51 Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.

25:1 "Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.

25:2 Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.

25:3 Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.

25:4 Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.

25:5 Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.

25:6 Usiku wa manane kukawa na kelele: Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.

25:7 Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.

25:8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.

25:9 Lakini wale wenye busara wakawaambia, Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!

25:10 Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa.

25:11 Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: Bwana, bwana, tufungulie!

25:12 Lakini yeye akawajibu, Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."

25:13 Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.

25:14 "Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng'ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.

25:15 Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.

25:16 Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.

25:17 Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.

25:18 Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.

25:19 "Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.

25:20 Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.

25:21 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.

25:22 "Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.

25:23 Bwana wake akamwambia, Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.

25:24 "Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya.

25:25 Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.

25:26 "Bwana wake akamwambia, Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.

25:27 Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!

25:28 Basi, mnyang'anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.

25:29 Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.

25:30 Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.

25:31 "Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,

25:32 na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.

25:33 Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.

25:34 "Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

25:35 Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;

25:36 nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.

25:37 Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?

25:38 Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?

25:39 Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?

25:40 Mfalme atawajibu, Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.

25:41 "Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.

25:42 Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.

25:43 Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.

25:44 "Hapo nao watajibu, Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?

25:45 Naye atawajibu, Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.

25:46 Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele."

26:1 Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,

26:2 "Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe."

26:3 Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, Kuhani Mkuu.

26:4 Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.

26:5 Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu.

26:6 Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma,

26:7 mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani.

26:8 Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, "Ya nini hasara hii?

26:9 Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha."

26:10 Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema.

26:11 Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.

26:12 Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko.

26:13 Nawaambieni kweli, popote ambapo hii Habari Njema itahubiriwa ulimwenguni, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye."

26:14 Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu,

26:15 akawaambia, "Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?" Wakamhesabia sarafu thelathini za fedha;

26:16 na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.

26:17 Siku ya kwanza kabla ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, "Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?"

26:18 Yeye akawajibu, "Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie: Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu."

26:19 Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka.

26:20 Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.

26:21 Walipokuwa wakila, Yesu akasema, "Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti."

26:22 Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, "Bwana! Je, ni mimi?"

26:23 Yesu akajibu, "Atakayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.

26:24 Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa."

26:25 Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, "Mwalimu! Je, ni mimi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema."

26:26 Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni mle; huu ni mwili wangu."

26:27 Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa akisema, "Nyweni nyote;

26:28 maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.

26:29 Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu."

26:30 Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.

26:31 Kisha Yesu akawaambia, "Usiku huu wa leo, ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.

26:32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya."

26:33 Petro akamwambia Yesu "Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe."

26:34 Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu."

26:35 Petro akamwambia, "Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe." Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.

26:36 Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali."

26:37 Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko.

26:38 Hapo akawaambia, "Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami."

26:39 Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: "Baba yangu, kama inawezekana, aacha kikombe hiki cha mateso kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe."

26:40 Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, "Ndiyo kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

26:41 Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i tayari lakini mwili ni dhaifu."

26:42 Akaenda tena mara ya pili akasali: "Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kinipite bila mimi kukinywa, basi, mapenzi yako yafanyike."

26:43 Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi.

26:44 Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale.

26:45 Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, "Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi.

26:46 Amkeni, twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti."

26:47 Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu.

26:48 Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha wapa ishara akisema: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni."

26:49 Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, "Shikamoo, Mwalimu!" Kisha akambusu.

26:50 Yesu akamwambia, "Rafiki, fanya ulichokuja kufanya." Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.

26:51 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

26:52 Hapo Yesu akamwambia, "Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga.

26:53 Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

26:54 Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?"

26:55 Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, "Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa Hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata!

26:56 Lakini haya yote yametendeka ili Maandiko ya manabii yatimie." Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.

26:57 Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokusanyika walimu wa Sheria na wazee.

26:58 Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa Kuhani Mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.

26:59 Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumwua,

26:60 lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,

26:61 wakasema, "Mtu huyu alisema: Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu."

26:62 Kuhani Mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, "Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?"

26:63 Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani Mkuu akamwambia, "Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, twambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!"

26:64 Yesu akamwambia, "Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa Mwenyezi, akija juu ya mawingu ya mbinguni."

26:65 Hapo, Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akasema, "Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake.

26:66 Ninyi mwaonaje?" Wao wakamjibu, "Anastahili kufa!"

26:67 Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi,

26:68 wakasema, "Haya Kristo, tutabirie; ni nani amekupiga!"

26:69 Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, "Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya."

26:70 Petro akakana mbele ya wote akisema, "Sijui hata unasema nini."

26:71 Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, "Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti."

26:72 Petro akakana tena kwa kiapo: "Simjui mtu huyo."

26:73 Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, "Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha."

26:74 Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, "Simjui mtu huyo!" Mara jogoo akawika.

26:75 Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: "Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." Basi, akatoka nje akalia sana.

27:1 Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.

27:2 Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.

27:3 Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha.

27:4 Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako."

27:5 Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.

27:6 Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu."

27:7 Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

27:8 Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.

27:9 Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei,

27:10 wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza."

27:11 Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema."

27:12 Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.

27:13 Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?"

27:14 Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.

27:15 Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.

27:16 Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.

27:17 Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwae Kristo?"

27:18 Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.

27:19 Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake."

27:20 Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

27:21 Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!"

27:22 Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!"

27:23 Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!"

27:24 Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe."

27:25 Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!"

27:26 Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe.

27:27 Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.

27:28 Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.

27:29 Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!"

27:30 Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.

27:31 Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.

27:32 Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.

27:33 Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa,"

27:34 wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.

27:35 Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.

27:36 Wakaketi, wakawa wanamchunga.

27:37 Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi."

27:38 Wanyang'anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.

27:39 Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,

27:40 "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!"

27:41 Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,

27:42 "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.

27:43 Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka."

27:44 Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.

27:45 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza.

27:46 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"

27:47 Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya."

27:48 Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.

27:49 Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa."

27:50 Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.

27:51 Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

27:52 makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;

27:53 nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.

27:54 Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu."

27:55 Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.

27:56 Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.

27:57 Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.

27:58 Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.

27:59 Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani,

27:60 akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.

27:61 Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.

27:62 Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,

27:63 Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, Baada ya siku tatu nitafufuka.

27:64 Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali."

27:65 Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo."

27:66 Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.

28:1 Baada ya Sabato, karibu na mapambazuko ya siku ile ya Jumapili, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kutazama lile kaburi.

28:2 Ghafla kutatokea tetemeko kubwa la nchi; malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akalivingirisha lile jiwe, akalikalia.

28:3 Alionekana kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.

28:4 Walinzi wa lile kaburi wakatetemeka kwa hofu kubwa, hata wakawa kama wamekufa.

28:5 Lakini yule malaika akawaambia wale wanawake, "Ninyi msiogope! Najua kwamba mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa.

28:6 Hayupo hapa maana amefufuka kama alivyosema. Njoni mkaone mahali alipokuwa amelala.

28:7 Basi, nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba amefufuka kutoka wafu, na sasa anawatangulieni kule Galilaya; huko mtamwona. Haya, mimi nimekwisha waambieni."

28:8 Wakiwa wenye hofu na furaha kubwa, hao wanawake walitoka upesi kaburini, wakakimbia kwenda kuwaambia wanafunzi wake.

28:9 Mara, Yesu akakutana nao, akawasalimu: "Salamu." Hao wanawake wakamwendea, wakapiga magoti mbele yake, wakashika miguu yake.

28:10 Kisha Yesu akawaambia, "Msiogope! Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, na huko wataniona."

28:11 Wale wanawake walipokuwa wanakwenda zao, baadhi ya walinzi wa lile kaburi walikwenda mjini kutoa taarifa kwa makuhani wakuu juu ya mambo yote yaliyotukia.

28:12 Basi, wakakutana pamoja na wazee, na baada ya kushauriana, wakawapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha

28:13 wakisema, "Ninyi mtasema hivi: Wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba sisi tukiwa tumelala.

28:14 Na kama mkuu wa mkoa akijua jambo hili, sisi tutasema naye na kuhakikisha kuwa ninyi hamtapata matatizo."

28:15 Wale walinzi wakazichukua zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Habari hiyo imeenea kati ya Wayahudi mpaka leo.

28:16 Wale wanafunzi kumi na mmoja walikwenda Galilaya kwenye ule mlima aliowaagiza Yesu.

28:17 Walipomwona, wakamwabudu, ingawa wengine walikuwa na mashaka.

28:18 Yesu akaja karibu, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

28:19 Nendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu; mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.

28:20 Wafundisheni kushika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote; naam, mpaka mwisho wa nyakati."


Next: Mark